dc.description.abstract | Utafiti huu ulihusu usawiri wa mwanamke katika nyimbo za sifo za jamii ya Wakamba. Ulikusudia kuchunguza iwapo mwanamke anadunishwa katika nyimbo hizi, anadunishwa vipi na iwapo anatetewa katika jamii dhidi ya imani dunishi za mfumo-dume. Duniani mwanamke hudharauliwa na kudunishwa kwa sababu ya jinsia yake. Imani hii dunishi imo katika itikadi na tamaduni zinazohimiliwa na mfumo-dume unaompa thamani kubwa mwanamume huku ukimdhalilisha mwanamke. Imani hii dunishi ni pamoja na kuozwa mapema, kuonewa kwa wanawake tasa, kunyimwa nyenzo za kujiendeleza miongoni mwa nyingine. Kwa hivyo, utafiti huu ulichunguza usawiri wa mwanamke katika nyimbo teule kumi ambazo ni: Ngungu na muoi (Tasa na mchawi) wa Kakai Kilonzo, Nyinyia wa Ndetei (Mama wa Ndetei) wa Kijana Mumo, Kavola Kamengele (Polepole Kamengele) wa Ancent Munyambu, Nyinyia Wa Syana (Mama Watoto) wa Dickson Mulwa, Mother (Mama) na Kana Nzula (Mpenzi Nzula) za Bosco Mulwa, Aka (Wanawake) wa Justus Myello, Aka ma town (Wanawake wa mjini) wa Danny Mutuku, Aka ni ma mithemba (Aina mbalimbali za wanawake) wa Wanginga na Syoka mami (Rudi mama) wa John Muasa. Utafiti ulihakiki nafasi ya mwanamke katika jamii na jinsi anavyosawiriwa katika nyimbo hizi. Tulitumia nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika ilioasisiwa na Filomena Steady. Nadharia hii ilitokana na ufeministi wenyewe ili kuhakiki masuala ya ufeministi katika jamii yenye utamaduni wa Kiafrika. Madai ya nadharia hii ni kutambua uwezo wa mwanamke, ukombozi wa wanawake na mwito wa kuwapa wanawake nafasi sawa na wanaume katika nyanja za kijamii, kisiasa, kielimu, kiuchumi na kidini katika muktadha wa jamii inayotawaliwa na ubabedume. Utafiti huu ulihusisha ukusanyaji wa kimakusudi wa sampuli kutoka maduka ya kuuza kanda za video mjini Machakos. Sampuli hii ilijumuisha nyimbo kumi (10) za watunzi tisa (9) wa kiume pekee ili kuchunguza mchango wao katika suala hili la ukombozi wa mwanamke. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa kutumia uchanganuzi elezi na takwimu elezi. Utafiti ulibaini kuwa watunzi wa nyimbo hizi za sifo za Wakamba wamemsawiri mwanamke kwa njia zilizo chanya japo kuna wale waliomsawiri kwa njia hasi. Matarajio yetu ni kuwa utafiti huu utasaidia jamii kubadilisha maoni yao na inavyodhaniwa kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii. Pia utachangia katika taaluma ya fasihi simulizi na fasihi simulizi ya jamii ya Wakamba. Walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za upili watafaidika na utafiti huu. | en_US |