• Login
    View Item 
    •   MKSU Digital Repository Home
    • Projects, Theses and Dissertations
    • MKSU Masters Theses
    • MKSU Masters Theses
    • View Item
    •   MKSU Digital Repository Home
    • Projects, Theses and Dissertations
    • MKSU Masters Theses
    • MKSU Masters Theses
    • View Item
    JavaScript is disabled for your browser. Some features of this site may not work without it.

    MABADILIKO YA KISEMANTIKI YA MANENO KATIKA LUGHA YA KIKAMBA: MTAZAMO WA KIDAYAKRONIA

    Thumbnail
    View/Open
    Thesis (1.541Mb)
    Date
    2025-11
    Author
    ANGELA NTHENYA MUSYOKA
    Metadata
    Show full item record
    Abstract
    Utafiti huu ulichunguza mabadiliko ya kisemantiki ya maneno ya Kikamba kwa mtazamo wa kidayakronia. Ulitalii jinsi maneno ya Kikamba yalivyobadilika maana kuanzia mwishoni mwa karne ya ishirini (20) (miaka ya sabini) hadi karne ya 21. Aidha, ulichunguza sababu za mabadiliko hayo. Uchunguzi ulifanywa kaunti ndogo ya Mwala katika Kaunti ya Machakos ukiwalenga wazungumzaji wa lahaja ya Ki᷉masaku. Hii ndiyo lahaja ambayo mtafiti pamoja na wakazi wengi wa kaunti ndogo ya Mwala huzungumza. Utafiti uliongozwa na nadharia mbili: Nadharia ya Dhana ambayo inashikilia kwamba maana ya neno ni dhana au taswira inayoibuliwa na neno hilo akilini mwa mwanalugha wakati neno hilo linapotamkwa; na Nadharia ya Nyanja za Kisemantiki inayoeleza kwamba maneno hayafai kuchukuliwa kama vipashio huru vinavyojitegemea, bali yanafaa kuhusishwa na mengine yanayohusiana kimaana. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza nomino na vitenzi ambavyo vimebadilika maana, kubainisha mabadiliko ya kisemantiki katika maneno hayo, kutathmini michakato ya kisemantiki inayohusishwa na mabadiliko hayo na kuchunguza sababu za mabadiliko hayo ya maana katika maneno ya Kikamba. Ukusanyaji wa data ulifanywa kwa kutumia mbinu ya mahojiano na ya maktabani. Maneno yalikusanywa kutoka Biblia za Kikamba; Mbivilia (UBS, 1974) na Mbivilia ya Ki᷉kamba kya Ivinda Yi᷉i᷉ (IT, 2011). Vitabu vinne (4) vya Biblia viliteuliwa kwa kutumia usampuli wa makusudi: Mwanzo na Zaburi katika Agano la Kale na Luka na Mathayo katika Agano Jipya. Maneno mia mbili (200) yaliteuliwa kimakusudi kutoka kwenye Biblia hizi mbili; nomino mia moja na kumi na sita (116) na vitenzi themanini na vinne (84). Fomyula ilitumiwa kupunguza maneno haya hadi hamsini (50). Mtafiti aliteua nomino thelathini (30) kimakusudi, kumi na tano (15) kutoka Mbivilia (1974) na kumi na tano (15) kutoka Mbivilia ya Ki᷉kamba kya Ivinda Yi᷉i᷉(2011). Vilevile, vitenzi ishirini (20) viliteuliwa kimakusudi, kumi (10) vikitolewa kwenye Mbivilia (1974) na kumi (10) kwenye Mbivilia ya Ki᷉kamba kya Ivinda Yi᷉i᷉(2011). Wahojiwa walikuwa wanaume watano (5) na wanawake watano (5) wenye umri wa miaka sabini na mitano (75) na zaidi na wavulana watano (5) na wasichana watano (5) ambao umri wao ni kati ya miaka kumi (10) hadi kumi na minne (14). Wote waliteuliwa kwa njia ya makusudi. Wazee hawa walijua maana ya maneno hayo kwa kuwa wameishi katika kipindi kinachotafitiwa na ndio mashahidi wa mabadiliko ya kisemantiki ya maneno ya Kikamba kuanzia mwishoni mwa karne ya 20 hadi karne ya 21. Data ilichanganuliwa kwa kulinganisha majibu ya wahojiwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo kwa kuzingatia malengo ya utafiti. Matokeo ya utafiti huu yatawasaidia wasomaji wa matini za Kikamba kuelewa maana za maneno kama yalivyotumika katika Biblia za awali hasa Biblia iliyochapishwa mwaka wa 1974 na maana mpya ya maneno hayo kwa mujibu wa Biblia iliyochapishwa mwaka 2011. Yataongezea tafiti zilizopo za kiisimu hasa kuhusu mabadiliko ya maana ya maneno katika lugha. Ni matumaini ya mtafiti kwamba kizazi cha sasa kitaelewa maana za maneno yanayopatikana katika matoleo ya awali ya Biblia ya Kikamba.
    URI
    http://ir.mksu.ac.ke/handle/123456780/20021
    Collections
    • MKSU Masters Theses [146]

    DSpace software copyright © 2002-2015  DuraSpace
    Contact Us | Send Feedback
    Theme by 
    @mire NV
     

     

    Browse

    All of Digital RepositoryCommunities & CollectionsBy Issue DateAuthorsTitlesSubjectsBy Submit DateThis CollectionBy Issue DateAuthorsTitlesSubjectsBy Submit Date

    My Account

    LoginRegister

    DSpace software copyright © 2002-2015  DuraSpace
    Contact Us | Send Feedback
    Theme by 
    @mire NV