dc.description.abstract | Lengo la kila mwandishi wa kazi ya fasihi ni kufikisha ujumbe kwa msomaji. Ili
kuwasilisha ujumbe huo kikamilifu, inambidi mwandishi atumie mbinu za kisanii
mbalimbali. Mbinu za kisanii hujumuisha jinsi masimulizi hufanywa kupitia kwa
wahusika, mbinu za uandishi, mandhari na lugha. Mandhari ni mojawapo ya kipengele cha
mbinu za kisanii ambacho hudokeza mahali matukio ya hadithi au masimulizi hutokea.
Kila jambo linalotendeka katika jamii hutendeka mahali fulani na kazi za kifasihi nazo
hufanya vivyo hivyo. Mandhari huweza kuwa halisi au ya kidhanifu. Mandhari na ujumbe
hutegemeana kwa kuwa mtunzi asiposawiri mandhari vilivyo, ujumbe hauwezi
kuwasilishwa kwa msomaji kikamilifu. Kwa mfano anapoeleza ujumbe kuhusu wanyonge,
lazima atumie mandhari duni kama vile mitaa ya mabanda. Azma ya utafiti huu ni
kuchunguza mchango wa mandhari ifaayo ili kufanikisha ujumbe wa mwandishi katika
riwaya mbili za Kiswahili Rosa Mistika (Kezilahabi) na Maisha Kitendawili (Habwe).
Riwaya hizi zilichaguliwa kupitia usampuli wa kimakusudi na zimeandikwa na waandishi
tofauti, mmoja wa nchi ya Tanzania na mwingine wa Kenya. Pia riwaya hizi ziliandikwa
miaka ya 1971 na 2000 mtawalia. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya uhalisia. Nadharia
ya uhalisia inadai kuwa msanii anatarajiwa kutoa picha za matukio na mazingira halisi
ambayo yanaonekana ili kuchora maisha kama yalivyo katika jamii. Kazi hii ilikuwa na
malengo haya: kwanza, kubainisha mandhari mbalimbali yaliyochorwa na waandishi. Pili,
kuchunguza mchango wa mandhari katika kufanikisha ujumbe wa mwandishi. Mwisho,
kutathmini ikiwa mandhari yaliyotumiwa na waandishi yameakisi hali halisi ya jamii.
Utafiti huu umekuwa wa maktabani na data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa kuzingatia
mihimili ya nadharia na matokeo yamewasilishwa kimaelezo. Utafiti uligundua kuwa
mandhari ni muhimu sana kwa mwandishi kuwasilisha ujumbe wake kikamilifu.
Matumaini ya mtafiti ni kuwa utafiti huu utakuwa na manufaa kwa wahakiki, wasomi na
walimu, wakuza mitaala na wanafunzi wa vyuo vikuu. Vilevile utachangia katika taaluma
ya uhakiki na fasihi ya Kiswahili kwa jumla. | en_US |